JE “BIFU” ZINASAIDIA WASANII?
Historia ya muziki wa kizazi kipya haiwezi
kukamilika pasipo kutaja matukio ya uhasama kati ya baadhi ya wasanii wa muziki
huo.Pengine neno ‘uhasama’ halileti ladha ama kuzua hisia zaidi katika ulimwengu
wa mziki wa kizazi kipya.Neno ‘bifu’, linalotokana na ‘beef’ ambalo ni
slang ya Kiingereza cha Wamarekani Weusi,
ni neno ambalo wengi hulitumia kuashiria uhasama kati ya wanamziki hususan wa
kizazi kipya hapa mombasani.
Mwandishi mmoja wa gazeti la Daily Mail la Uingereza
aliwahi kuandika kuwa ‘vituko katika fani ya muziki wa hip-hop na rap ni
miongoni mwa chembechembe muhimu kwa mafanikio ya msanii wa muziki huo’. Alitaja
vituko hivyo kuwa ni pamoja na bifu. Iwapo bifu zinasaidia uhai wa hip-hop na
rap au zinadidimiza, mie sina jibu bali kwa namna moja au nyingine zimewasaidia
baadhi ya wasanii kufanya vizuri katika mauzo ya albamu zao.
Katika mjadala wa kubainisha iwapo bifu ama
uhasama baina ya wasanii husadia ama kutosaidia kukua kwa sanaa ya mziki
mombasani, washikadau wakuu wa mziki wa kizazi kipya (mashabiki) wachora
mitazamo tofauti.
WALIOUNGA MKONO.
Katika Kipindi cha Chipkizi Za Kaya Jumapili
iliyopita Walioegemea mtazamo kwamba bifu husaidia wa hoji kwamba tabia ya
uhasama baina ya wasanii ni utamaduni wajadi hususan katika ulimwengu wa mziki
wa Hiphop. Uhasama huu watajwa kuongeza umaarufu wa wasanii husika kwani
waskilizaji hugawanyika na kuamua ni yupi kati ya wasanii wawili wanaolumbana
watawashabikia. Hii huzua na kujenga mashabiki sugu wa wasanii husika, ambao
wanaweza kufananishwa na mashabiki sugu wa timu za soka. Kuna imani miongoni
mwa baadhi ya wapenzi wa hip-hop na rap kwamba bifu kati ya wasanii marehemu
Tupac Shakur na Notorious B.I.G ilisaidia sana kuongeza umaarufu wa wasanii
hao.
Bila shaka wafuatiliaji wa bongoflava wanakumbuka
bifu kati ya Juma Nature na Inspekta Haroun na ile ya wasanii wa East Coast
Team na wale wa maeneo ya Temeke. Japo haifahamiki vizuri historia ya bifu hizo
mbili, lakini kwa hakika zilivuta hisia za wapenzi wengi wa bongoflava.Hapa mombasani mbali na kupanda kwa joto la
kisiasa mwaka wa 2007 uhasama kati ya wasaani waliokua juu nyakati hizo
Rudeboys na msanii aliyekua anachipuka Susumila yatajwa kuchangia kupanda kwa
umaarufu wa Susumila miongoni mwawakereketwa wa fani ya Mombasani. Jijini Nairobi
kupanda kwa umaarufu wa Octopizzo watajwa kuchangiwa sana na uhasama baina yake
na msanii mkongwe wahiphop Abbas Kubaff, huku bifu kati ya Bamboo na wafuasi wa
kundi la Klepto pia latajwa kuchangia kutambulika kwa baadhi ya wasanii wa
kundi hilo.
Tabia hii pia yatajwa kuongeza mauzo ya album
katika mataifa yaliyoendelea. Bifu kati ya msanii Rick Ross na 50 Cent nchini
marekani inaaminika kuchangia mauzo mazuri ya albmu ya Rick Ross inayofahamika
kama ‘Deeper Than Rap‘.
Hata hivyo,kama kweli bifu zinasaidia
maendeleo ya wasanii, kwanini basi marapa kama Ja Rule na Fat Joe ‘wamepotea’
licha ya bifu lao na 50 Cent huku Benzino akibaki historia baada ya bifu lake
na Eminem?Au ili bifu lizae matunda ‘yanayokusudiwa’ sharti wahusika
‘waimudu’(kama Rick Ross alivyoweza ‘kustahimili’ bifu lake na 50 Cent)?Lakini
kama suala ni ‘kumudu bifu’ mbona Jadakiss ameweza ‘kusimama vizuri’ hata baada
ya ‘kupatana’ na 50 Cent?
Wakichangia mjadala huu katika kipindi cha
Chipkizi za Kaya, baadhi ya wasikilizaji pia wasema amani haiji ila kwa ncha ya
upanga na kinachofuata baada ya uhasama huu
huwa mapatano na heshima. Uwepo wa heshma katika sanaa ya mziki
kunachangia kukua kwa mziki kwani mipaka baina ya wasanii mbali mbali huwa wazi
na kazi zao ndizo zinazowawakilisha kwa mashabiki wao.
WALIOPINGA;
Msemo wa umoja ni nguvu na utengano ni
udhaifu ulikua kauili mbiu ya wengi waliopinga kwamba uhasama husaidia sanaa ya
mziki wa kizazi kipya. Bifu yatajwa kuleta mgawanyiko si kwa wasanii wahusika
pekee, bali hata kwa mashabiki. Hali hii yatajwa kusabaratisha baadhi ya wasanii
na kupeana nafasi kwa wasanii wachache kupata mafanikio ya kimziki pekee kwa
mda mrefu.
Kusambaratika kwa kundi la ECT na TMK baada
ya bifu yao kwatajwa kama mfano. Bifu kati ya wasanii wa iliyokuwa East Coast
Team na wale wa Temeke ilikufa kitambo kama ilivyotokea kwa bifu kati ya Nature
na Inspekta. Lakini cha kushangaza, sio tu kwamba bifu hizo zilikwisha bali pia
kulijitokeza mabadiliko makubwa kuhusu wasanii waliohusika na bifu hizo.
East Coast Team ilisambaratika huku wanakundi
MwanaFA na AY wakitangaza kufanya kazi zao za kisanii kibinafsi (na wameendelea
kuwa na mafanikio makubwa) lakini majina kama King Crazy GK (kiongozi wa kundi
hilo) na O’Ten yamebaki kuwa historia tu.Kwa wenzao wa Temeke, japo kulizuka
bifu jingine kati ya Wanaume Family na Wanaume Halisi baada ya kundi la Wanaume
kugawanyika, kinachoweza kupigiwa mstari zaidi ni ‘kupotea’ kwa Nature na
Inspekta katika anga za bongofleva.Ikumbukwe kuwa wasanii hao wawili walifikia
hatua ya kupatana bbadaye na kushirikiana katika kundi la Wanaume Halisi.
Wanaoshuku mtazamo kwamba bifu hupelekea
kupanda kwa mauzo ya album za wasanii wahusika wapiga mfano wa kudorora kwa
mauzo ya album ya 50 Cent ya ‘Before I Self Destruct‘ licha ya uwepo wa bifu kubwa na msanii
mwengine Rick Ross?
Udogo wa game ya Mombasani pia watajwa
kutoweza kuwafanikisha wasanii wenye bifu. Uchache wa mashabiki wazua ugumu wa
kuwaganya kwani hata wakigawanywa wale ambao msanii atawapata hawawezi
kumfaidisha.Kutokuwa na utamaduni wa mashabiki kununua
album madukani ama kupitia mtandao pia kwatajwa kutowafaidisha wenye bifu kwani
uhasama wao hutajwa tu maredioni na hakutakua na faida kwao. Pia mashabiki wasema
Ifikiapo hapa huhitajika utayari wa washikadau wa vyombo vya habari kuzungumzia
bifu hili kuwafikia mashabiki lakini isipokuwa hivi, bifu hili huishia mitaani
likijulikana na wasanii wenyewe tu na marafikizao wa karibu.
Wengine wasema ili ufanisi upatikane kutokana
na bifu, kunahaja ya wasanii wote kuhusika vilivyo katika uhasama huo. Msanii
mmoja anapompuuza mwengine na kuamua kutomjibu mwenzake katika malumbano
hususan ya nyimbo na katika mahojiano, hupunguza makali ya mchakato mzima wa
bifu na kupunguza utamu. Kutojibiwa kwa msanii Daddy Q na msanii susumila wakati
bifu baina yao Mombasani kwatajwa kutompa nafasi Daddy Q kupata umaarufu, huku
hatua ya rudeboyz kumjibu susumila kukionekena kama hatua iliyosaidia kupatikana
kwa umarufu kwa uhasama baina yao na pia kusambaa kwa jina la msanii susumila.
Je kufikia hapa inatosha kusema kuwa bifu ni
jambo jema au baya kwa sanaa ya muziki? Mie nimechokoza mjadala tu, nakuachia wewe
msomaji uuendeleze nauamue.
Kwa mengi Zaidi usikose kumskiza Sista Shaniz
a.k.a Anti-Virus katika "Show Nambari Moja Mkoani Pwani™" -
"Kaya Flavaz®" ndani ya RADIOKAYA 93.1Fm Msa 99.7Mlnd - "Kitovu
Cha Umoja Wa Pwani ™.
©mwanamgambo2012